Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA – Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Urusi, Kazem Jalali, ametangaza kuwa mji wa Qazan, ambao ni makao makuu ya Jamhuri ya Tatarstan, umeongezwa rasmi katika orodha ya miji itakayokuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Wiki ya Utamaduni wa Iran Nchini Urusi.
Jalali alisema kuwa maadhimisho hayo ya kitamaduni yatafanyika katika miji ya Qazan, St. Petersburg na Moscow, yakilenga kuonesha urithi wa ustaarabu wa Iran na kuimarisha mawasiliano ya kitamaduni kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
Akizungumza katika kikao chake na Mkuu wa Maktaba ya Taifa ya Urusi, Jalali alibainisha kuwa Wiki ya Utamaduni wa Iran itatoa fursa muhimu ya kukuza mazungumzo ya kitamaduni na kupanua ushirikiano katika sekta za maktaba, elimu na utamaduni.
Aidha, balozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kitamaduni kati ya Iran na Urusi. Alieleza kuwa Ubalozi wa Iran uko tayari kuunda kikosi kazi cha pamoja cha watafiti kutoka pande zote mbili kwa ajili ya kufanya tafiti na kuandika upya historia ya mahusiano ya Iran na Urusi kwa kutegemea nyaraka rasmi za nchi hizo mbili.
Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Tehran na Moscow ya kuendeleza diplomasia ya utamaduni na kuimarisha uhusiano wa kihistoria kupitia tafiti, elimu na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma
Maoni yako